Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezindua rasmi dirisha la maombi ya Samia Extended Scholarship Programme kwa wahitimu wa kidato cha sita mwaka 2025, hususan wale waliobobea katika masomo ya sayansi na hisabati ya juu.
Mpango huu wa udhamini kamili unalenga kuandaa kizazi kipya cha wataalamu wa Data Science, Artificial Intelligence (AI), na Sayansi ya Kompyuta, kwa ajili ya kuchochea uchumi wa kidijitali nchini.
Wahitimu wa kidato cha sita nchini sasa wana nafasi ya kujiendeleza kielimu kupitia Samia Scholarship, mpango wa kitaifa wa ufadhili wa masomo ulioanzishwa kwa lengo la kuendeleza vipaji na kuimarisha maendeleo ya rasilimali watu nchini.
Dirisha la maombi kwa mwaka huu limefunguliwa rasmi, na wahitimu wanahimizwa kuwasilisha maombi yao kabla ya tarehe ya mwisho. Ufadhili huu unalenga wanafunzi wenye ufaulu wa juu kutoka familia zisizo na uwezo mkubwa kiuchumi, huku ukisisitiza masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi, na hisabati (STEM).
📌 Vigezo vya Kuomba:
- Kuwa mhitimu wa kidato cha sita mwaka 2025
- Kuwa na ufaulu wa juu (division one au two)
- Kutoka familia yenye kipato cha chini
- Kuonyesha nia ya kusoma masomo ya STEM, afya, au fani za kiufundi.
- Wahitimu 700 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wanastahiki kuomba.
- Wanafunzi 50 bora watashiriki bootcamp ya miezi 10 katika NM-AIST kabla ya kujiunga na vyuo vikuu vya kimataifa kama MIT (Marekani), Oxford (Uingereza), IIT Madras (India), na Peking (China).
- Wanafunzi 650 waliobaki watasoma katika taasisi maalumu za sayansi na teknolojia ndani ya Tanzania.
📥 Jinsi ya Kuomba:
Wanafunzi wanaweza kuwasilisha maombi yao kupitia tovuti rasmi ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo (NACTVET) au kupitia www.samia-scholarship.go.tz ,. Maombi yote yanapaswa kuambatanishwa na vyeti halali vya matokeo na barua ya utambulisho kutoka serikali za mitaa.
Mpango huu unasimamiwa na COSTECH kwa kushirikiana na NM-AIST, Watanzania waishio nje ya nchi, na washirika wa kimataifa. Prof. Maulilio Kipanyula, Makamu Mkuu wa Chuo cha NM-AIST
, alieleza kuwa huu si udhamini tu, bali ni "uwekezaji wa kizalendo kwa mustakabali wa Tanzania."
Wadau wa elimu nchini wamepongeza juhudi hizi wakisisitiza kuwa
Samia Scholarship ni chombo thabiti cha kuibua kizazi kipya cha wataalamu wa fani mbalimbali, hususan maeneo ya kimkakati kama afya, mazingira, na teknolojia.


0 Comments
Post a Comment